1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Helikopta ya jeshi la Kenya yaanguka Somalia

Grace Kabogo
19 Septemba 2023

Helikopta ya jeshi la Kenya imeanguka karibu na mpaka wa Somalia na kusababisha vifo vya watu wapatao wanane.

https://p.dw.com/p/4WYwp
Somalia African Union Soldaten
Picha: Ed Ram/Getty Images

Taarifa ya jeshi imeeleza kuwa helikopta hiyo ya kikosi cha anga imeanguka ikiwa katika doria usiku. Imesema timu ya ya wachunguzi imepelekwa kwenye eneo la tukio.

Haijafahamika mara moja kilichosababisha ajali hiyo iliyotokea kwenye kaunti ya Lamu, pwani ya Kenya.

Maafisa wa jeshi na polisi ambao hawakutaka kutajwa jina, wamesema wanajeshi wote na wafanyakazi wa helikopta hiyo waliokuwemo ndani, wamekufa.

Soma: Wasiwasi watanda Somalia kuondoka kwa kikosi cha Umoja wa Afrika

Vikosi vya ulinzi vya Kenya vinaendesha shughuli zake kwenye eneo hilo katika juhudi za kupambana na kundi la Al-Shabaab lenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaida.

Wanajeshi wa Kenya pia wako Somalia chini ya kikosi cha mpito cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS).