1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ruto aamuru jeshi kuwaokowa waliokumbwa na mafuriko

30 Aprili 2024

Rais William Ruto wa Kenya ameliagiza jeshi kuwahamisha wananchi ambao wamekumbwa na mafuriko baada ya watu 171 kufariki dunia kufuatia mvua kubwa zaidi kulikumba taifa hilo la Afrika mashariki tangu mwezi Machi.

https://p.dw.com/p/4fMm1
Mafuriko katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.
Mafuriko katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.Picha: Thomas Mukoya/REUTERS

Rais Ruto, ambaye aliwatembelea waathirika wa mkasa huo baada ya kuongoza kikao cha Baraza la Mawaziri mjini Nairobi, alisema serikali imechora ramani ya vijiji ambavyo vipo hatarini kukumbwa na mafuriko, wakati tahadhari ya mvua zaidi ikitolewa.

Waokoaji walikuwa wanaendelea kuitafuta miili ya waathirika baada ya mvua kusababisha mafuriko na maporomoko makubwa kabisa ya ardhi kuwahi kushuhudiwa kwenye taifa hilo la Afrika Mashariki katika miaka ya karibuni.

Soma zaidi: Waliokufa kwa mafuriko, maporomoko Kenya wapindukia 160

Taarifa zilisema kuwa idadi ya watu ambao hawajulikani walipo ilikuwa ikiendelea kuongezeka.

Zaidi ya watu 190,000 wameyakimbia makaazi yao wakiwemo 147,000 katika mji mkuu wa Nairobi, huku Idara ya Hali ya Hewa nchini himo ikisema bado maeneo kadhaa yalikuwa yakitarajiwa kupata mvua kubwa katika siku zijazo.