1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaombwa izuie hatua ya kuushambulia mji wa Rafah

Saumu Mwasimba
28 Aprili 2024

Saudi Arabia inakhofia vita kati ya Israel na wanamgambo wa Hamas vilivyoongeza mivutano katika kanda ya Mashariki ya kati vinaweza kuvuruga hali ya kiuchumi duniani kote

https://p.dw.com/p/4fGxp
Saudi Arabien Riad | Weltwirtschaftsforum
Picha: Thaer Ganaim/ZUMA/picture alliance

Saudi Arabia ambayo ni mwenyeji wa mkutano maalum wa kimataifa unaojadili masuala ya kiuchumi  imetowa mwito wa uthabiti katika kanda ya Mashariki ya kati, huku ikitahadharisha kuhusu athari zinazoweza kusababishwa duniani na vita vinavyoendelea kati ya Israel na wanamgambo wa Hamas.

Mtazamo wa Saudi Arabia umetolewa kwenye ufunguzi wa mkutano huo wa kilele unaohudhuriwa na mataifa mbali mbali. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken, viongozi wa mamlaka ya Wapalestina na maafisa wa ngazi za juu kutoka nchi nyingine wanaojaribu kuzishawishi pande hizo mbili kwenye mzozo zifikie makubaliano ya kusitisha vita wako kwenye orodha ya wageni wanaosshiriki mkutano huo wa Riyadh.

Viongozi wakishiriki mjadala wa WEF
Bola Ahmed Tinubu, Anwar Ibrahim na Kristalina Georgieva Picha: Fayez Nureldine/AFP

Katika kikao cha mwanzo cha mjadala kwenye mkutano huo wa siku mbili, waziri wa fedha wa Saudi Arabia,Mohammed al-Jadaan alisema vita vya Gaza pamoja na migogoro mingine ikiwemo Ukraine inachangia kusababisha shinikizo kubwa katika hali ya kiuchumi.

Akigusia zaidi kuhusu athari za vita vya Gaza waziri huyo amesema ni mgogoro uliosababisha mivutano ya kikanda kuongezeka na mataifa yenye nguvu pamoja na viongozi wanapaswa kuidhibiti hali hiyo.

Wito wa rais wa Mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas

Rais wa mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas ambaye pia anashiriki mkutano huo wa jukwaa la kiuchumi amesema Marekani ni nchi pekee inayoweza kuizuia hatua inayokhofiwa kwa muda mrefu kuchukuliwa na Israel ya kuuvamia mji wa Rafah,Kusini mwa Gaza.

Mahmoud Abbas ameiomba Marekani iizuie Israel kuendesha operesheni ya kijeshi katika mji huo akitahadharisha kwamba itasababisha uharibifu mkubwa na maafa kwa raia ambao tayari wameachwa bila makaazi.

Mkutano huo wa Riyadh hauhudhuriwi na mjumbe yoyote kutoka Israel. 

Riyadh mji mkuu wa Saudi Arabia
Mji wa kiuchumi wa Saudi Arabia wa RiyadhPicha: Sigrid Wolf-Feix/imageBROKER/picture alliance

Mbali na masuala ya migogoro mkutano huo wa kimataifa wa  Jukwaa la kiuchumi-WEF unaipa pia nafasi Saudi Arabia kuonesha mageuzi yake kwenye upande wa masuala ya kijamii ikiwemo kurudisha matukio ya burudani kama vile sinema pamoja na kuondowa marufuku ya wanawake kuendesha magari