1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUfaransa

Urusi yaionya Ufaransa fikra ya kupeleka wanajeshi Ukraine

4 Aprili 2024

Mawaziri wa Ulinzi wa Urusi na Ufaransa wamefanya mazungumzo ya nadra siku ya Jumatano ambapo Urusi imeitahadharisha Ufaransa dhidi ya kutuma wanajeshi wake nchini Ukraine.

https://p.dw.com/p/4ePGP
Waziri wa Ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu (kushoto) akiwa na Rais Vladimir Putin.
Waziri wa Ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu (kushoto) akiwa na Rais Vladimir Putin.Picha: ALEXANDER KAZAKOV/AFP

Mazungumzo hayo kwa njia ya simu kati ya Waziri wa Ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu na mwenzake wa Ufaransa Sebastien Lecornu ni ya kwanza baina ya viongozi hao wawili katika kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja na nusu.

Taarifa iliyotolewa na Moscow imesema Shoigu amemwaleza kinagaubaga Lecornu kwamba iwapo serikali mjini Paris itafuata matamshi yake ya juu ya uwezekano wa kutuma kikosi cha jeshi la Ufaransa nchini Ukraine, "hilo litasababisha matatizo kwa Ufaransa yenyewe."

Taarifa hiyo haikufafanua zaidi kuhusu maana ya tahadhari hiyo iliyotolewa na waziri Shoigu.

Hata hivyo suala hilo limeibuka kwenye mazungumzo baina ya viongozi hao wawili kufuatia matamshi ya Rais Emmanuel Macron aliyoyatoa mwezi Februari, ambapo alisema haondoi uwezekano kwa nchi za magharibi kutuma wanajeshi wake nchini Ukraine.

Matamshi hayo ya Macron yalizusha hamkani miongoni mwa washirika wa nchi za magharibi na viongozi kadhaa wa Ulaya ikiwemo Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani walijetenga mara moja na mtizamo huo.

Ufaransa yatoa mkono wa pole kwa shambulio lililoitikisa Moscow

Taarifa iliyotolewa na Ufaransa, imesema waziri Lecornu alitoa salamu za rambirambi kwa mwenzake wa Urusi na kulaani shambulio la kigaidi lililoutikisa mji mkuu Moscow mnamo mwishoni mwa mwezi Machi.

Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa, Sebastien Lecornu.
Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa, Sebastien Lecornu.Picha: JULIE SEBADELHA/AFP

Lecornu amemhakikishia Shoigu kuwa Ufaransa iko tayari kutanua ushirikiano wake na Urusi katika kupambana na ugaidi. Lakini pia Lecornu akasisitiza kuwa nchi yake haina taarifa juu ya uhusiano kati ya shambulizi dhidi ya ukumbi wa starehe wa Crocus huko kaskazini mgharini mwa Moscow na Ukraine.

Shambulio hilo liliwaua watu 139 na Urusi imesema inao ushahidi wa kuhusika kwa Ukraine kwenye mkasa huo. Kulingana na taarifa ya Ufaransa, waziri Lecornu amemrai mwenzake wa Urusi kutolitumia shambulio hilo kama msingi wa kufanya hujuma yoyote kwa Ukraine.

Imearifiwa vilevile, Lecornu amejaribu kuishawishi Moscow itambue Ukraine na nchi za magharibi hazihusiki na shambulio hilo la wiki za karibuni na kwamba pande hizo mbili zinalaani mkasa huo wa kigaidi unaoaminika kufanywa na kundi linalojiita Dola la Kiislamu.

Kwenye suala hilo upande wa Urusi umeripoti kuwa waziri Shoigu alimweleza Lecornu, "Utawala wa Kyiv haufanyi chcohote bila wapanga mipango wa nchi za magharibi. Kwenye hili tunaamini Ufaransa haikuhusika."

Mzozo wa Ukraine watawala majadiliano kwa kila upande kuvutia upande wake

Kwa mujibu wa serikali mjini Paris, waziri Lecornu ametumia mazungumzo hayo ya simu kulaani vita vya Urusi nchini Ukraine na kwamba amweleza Shoigu kuwa Ufaransa itaendelea kuiunga mkono Ukraine bila kuchoka.

Kifaru cha vita
Kifaru cha vitaPicha: Jose Colon/Anadolu/picture alliance

Kuhusu vita hivyo, imearifiwa Shoigu alizungumzia utayari wa Urusi wa "kufanya mazungumzo kuhusu Ukraine", akisisitiza kwamba duru ya mazungumzo ya amani iliyopangwa kufanyika mjini Geneva haitokuwa na maana iwapo Urusi haitahusika.

Amesema uwezekano wa mazungumzo katika siku zijazo unaweza kujumuisha kile rasimu iliyoandaliwa wakati wa mashauriano kati ya Urusi na Ukraine ya mwezi Machi mwaka 2022 mjini Istanbul, Uturuki.

Duru za habari zilisema rasimu hiyo inahusisha kipengele cha kutaka Ukraine iachane na mipango ya kujiunga na Jumuiya ya Kujihami ya NATO. Hakuna mwafaka uliopatikana wakati huo na mazungumzo hayo yalivunjika.

Hata hivyo Ufaransa imesema matamshi hayo ya Shoigu hayakuakisi msimamo wa serikali ya Paris. Chanzo kimoja ndani ya serikali ya Ufaransa kimesema "siyo kweli", kwamba Ufaransa imeonesha dhamira ya kufanyika mazungumzo kuhusu Ukraine.